CORONA (COVID 19) TANZANIA SERIKARI YATOA TAMKO

UDHIBITI WA CORONA, SERIKALI YATAJA MASHARTI YA KUFUATWA: Serikali imeamua kuimarisha udhibiti wa maambukizo ya virusi vya corona nchini hususan kwa wasafiri wa kimataifa kuanzia Mei 4 kwa kuzingatia mambo kadhaa ikiwemo kuzitaka mamlaka zote katika vituo vya kuingia nchini zinazingatia hatua za kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona kwa wasafiri na wafanyakazi wa maeneo hayo kwa kuosha mikono kwa kutumia sabuni na maji tiririka, kutumia vitakatishi mikono, kukaa kwa umbali unaoshauriwa na kuvaa barakoa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi wasafiri watatakiwa kujaza kwa uaminifu fomu iliyopo mtandaoni kuonyesha hali ya afya ya msafiri katika muda wa saa 24 kabla ya kuingia Tanzania na kuwataka wasafiri wote wageni na wakazi wanaorejea nchini kuwasilisha cheti kinachoonyesha kutokuwa na maambukizo ya ugonjwa wa COVID-19 na kipimo hicho kiwe katika mfumo wa RT-PCR kwa kutumia sampuli zilizochukuliwa ndani ya saa 72 kabla kuingia Tanzania.

Pia wasafiri wageni na wakazi wanapoondoka Tanzania watalazimika kupima maambukizo ya virusi vya corona ikiwa ni pamoja na kutumia kipimo cha haraka kwa wanaowasili nchini kutokea katika maeneo yenye maambukizo makubwa wakitozwa dola 25 kwa kila msafiri anayepata huduma hiyo.

Na kwa wasafiri wanaotoka katika nchi zenye Virusi vipya vya Corona kwa kuzingatia taarifa inayotolewa kila siku na Shirika la Afya Duniani(WHO) au kwa wale waliosafiri katika nchi hizo ndani ya siku 14 zilizopita kabla ya safari zao watapimwa kipimo cha haraka katika kituo cha kuingilia nchini na kulazimika kukaa karantini kwa siku 14 kwa gharama zao.

Na kwa upande wa malori na magari yanayovuka mipaka yatalazimika kuwa na watu wawili mpaka watatu ili kurahisisha utaratibu wa kuvuka mipaka.
Profesa Makubi amesema taarifa ya ushauri kwa wasafiri itapitiwa mara kwa mara kadiri inavyohitajika.

Leave a Comment