Mchungaji Jera Kwa Kurawiti Mtoto wa Miaka 4

Dar es Salaam. Mahakama ya Mkoa wa Kinondoni imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela Elisha Mushi (22), mkazi wa Ubungo Kibangu baada ya kuthibitika kumlawiti mtoto wa miaka minne kanisani.

Mushi, ambaye alikuwa akifanya kazi ya kufundisha watoto kanisani anadaiwa kutenda kosa hilo Februari 19, mwaka huu katika Kanisa la Embassy Kingdom.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Ester Mwakalinga baada ya kuwasikiliza mashahidi saba wa upande wa mashitaka, akiwamo mtoto mwenyewe, mama mzazi pamoja na mchungaji wa Kanisa la Embassy Kingdom aliyekiri kumfahamu mama mzazi wa mtoto aliyetendwa.

Mashahidi wengine ni daktari wa Hospitali ya Sinza Palestina aliyempima mtoto huyo pamoja na askari wa Kituo cha Polisi Osterbay. Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Ester alisema kutokana na ushahidi uliotolewa na mtoto mwenyewe pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa, mahakama imejiridhisha pasipo shaka yoyote kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa analotuhumiwa nalo.

“Kutokana na vielelezo vilivyowasilishwa, ikiwemo ripoti ya daktari (PF3) na ushahidi wa mama na mtoto mwenyewe, mahakama imejiridhisha pasipo shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo, hivyo inakutia hatiani kwa kosa la kulawiti,” alisoma Hakimu Ester.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Hilda Kato aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia ya kufanya vitendo vya udhalilishaji na kikatili kama hivyo katika jamii.

Hata hivyo wakati wa kujitetea, Mushi alisema hakuwahi kufanya kosa kama hilo na kuiomba mahakama imsamehe na kumwachia huru kwa kuwa yeye hahusiki kutenda kosa hilo.

Hakimu Ester alisema ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia za kikatili na za udhalilishaji kama hizo, mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela na kama hajaridhishwa na hukumu hiyo anayo haki ya kukata rufaa. Katika kesi ya misingi, inadaiwa kuwa Februari 19 katika Kanisa la Embassy Kingdom ambako mshitakiwa alikuwa akifanya kazi ya kuwafundisha watoto (Sunday school) alilawiti mtoto wa miaka minne kinyume cha sheria za nchi.

Leave a Comment