
Maafisa wa Colorado nchini Marekani wanasema mtu aliyewaua watu sita katika hafla ya siku ya kuzaliwa wikendi iliyopita alikasirika kwa kukosa kualikwa.
Polisi wanasema Teodoro Macias, 28, alimpiga risasi na kumuua mpenzi wake, Sandra Ibarra-Perez, 28, pamoja na jamaa zake watano kabla ya kujielekezea bunduki.
Kisa hicho kilitokea katika bustani ya Canterbury eneo la Colorado Spring mapema siku ya Jumapili.
Sherehe hiyo ilikuwa imeandaliwa jamaa watatu, na wawili kati yao wamefariki.
Shambulio hilo limetokea chini ya miezi miwili baada ya kisa cha ufyatuaji risasi kilichosababisha vifo vya watu 11 kwenye duka la mboga katika mji wa Boulder kaskazini-kati mwa Colorado.
Polisi wanasema mshambuliaji huyo wa Colorado “alizozana” na familia hiyo katika shughuli nyingine mapema wiki hiyo, na alikuwa mpenzi mwenye wivu.
“Katika kisa hiki cha kushangaza cha mzozo wa kinyumbani,” Afisa mkuu wa polisi wa Colorado Springs Vince Niski aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumanne na kuongeza: “Wakati [Macias] alipogundua hakualikwa katika hafala hiyo ya kifamilia, mshukiwa alijibu hatua hiyo kwa kuwashambulia kwa bunduki.”
Alisema mshukiwa alikuwa na “kadhia ya kushindwa kujidhibiti kutumia nguvu”, na amekuwa katika mahusiano na mpenzi wake kwa karibu mwaka mmoja. Hakuwa na rekodi ya uhalifu.
Vijana watatu waliondoka katika hafla hiyo kwenda kuchukua vitu kwa jirani yao muda mfupi kabla ya shambulio hilo kutokea na kurejea kwenye gari baada ya shambulio, Luteni wa polisi Joe Frabbiele aliwaambia wanahabari.
Watoto watatu, walio na umri wa miaka miwili, mitano na 11, walishuhudia kisa hicho, lakini hawakujeruhiwa, walisema polisi. Maganda 17 ya risasi yalipatikana katika eneo la tukio.
Siku ya Jumanne, polisi wa Colorado Springs waliwatambulisha ndugu watano walioawa kuwa ni:
- Melvin Perez, 30
- Joana Cruz, 53 (Mama yake Melvin)
- Jose Gutierrez Cruz, 21 (Kaka yake Melvin)
- Mayra Perez, 32 (Mke wa Melvin)
- Jose Ibarra (Kaka yake Mayra)
Nubia Marquez, dada yake Melvin Perez na binti wa Joana Cruz aliliambia gazeti la Colorado Springs kwamba watatu hao walikuwa wanaadhimisha siku zao ya kuzaliwa wiki moja “na wamekuwa wakipenda kusherehekea pamoja”.
Alihudhuria hafla hiyo nyumbani kwa familia ya Cruz iliyopo trailer park akiwa na mume wake, Freddy Marquez.
Lakini wanandoa hao waliwaambia wanahabari kwamba waliondoka karibu saa nne usiku wa Jumamosi.
Ufyatuaji risasi ulifanyika muda mfupi baada ya saa sita usiku.
Bw. Marquez alimkumbuka mama mkwe wake, na kuliambia Gazette kwamba mke wa Cruz alikuwa “kipenzi cha watu” na “mchapa kazi” mama wa watoto wanne ambaye alikuwa “mwenye furaha wakati wote” na amewalea watoto wake kuwa “watu wangwana”.
Bw. Marquez aliliambia Gazeti la Colorado Springs kwamba mshambuliaji alikuwa mtu “mpole” na mwenye “hasira” na wakati wote alikuwa na bunduki.
Kulingana na polisi, mshambuliaji hakuwa na idhini ya kisheria ya kumiliki bastola hiyo.
Katika taarifa siku ya Jumapili, Gavana wa Colorado, Jared Polis alilaani “kitendo hicho cha kikatili”, akisema kwamba kimetokea wakati “wengi wetu tulikuwa tunasherehekea siku ya wanawake walio katika maisha yetu na ambao wamechangia utu wetu “.